Kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wanachama, wadau na
makada wa CCM, kuondokana na unyonge, imepokewa kwa hisia tofauti huku
ikielezwa kuwa ni ya vitisho.
Juzi, wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM
mjini Dodoma, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho
tawala alisema: “Ni wakati wa kuacha unyonge na uvumilivu una kikomo
chake.”
Alisema CCM inaingia kwenye uchaguzi huku ikishindana na
wagomvi: “…Ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wao kufanya siasa,” alisema
Kikwete bila kutaja jina la chama chochote cha siasa.
Alisema amechoshwa na vitendo vya ugomvi huku akitolea
mfano wa tukio la Kahama mkoani Shinyanga ambako kijana mmoja alitolewa
macho kwa bisibisi na mwingine kumwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo
wa ubunge Igunga, mkoani Tabora.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe alieleza kushangazwa kwake na kauli ya Rais Kikwete akisema:
“Nimeipokea kwa mshtuko na ninawataka wafuasi wa chama changu kuwa
watulivu na kuchukua tahadhari kubwa.”
“Nilichokifanya ni kuwaagiza wafuasi wa Chadema kufanya
kampeni za kistaarabu kwa kutolipiza kisasi ili kuhakikisha kwamba
hakuna damu ya Mtanzania itakayomwagika Kalenga,” alisema.
Hatua ya Rais Kikwete, imekuja baada ya CCM kumtangaza,
Godfrey Mgimwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga. Mgimwa ni mtoto
wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha,
hayati Dk William Mgimwa aliyefariki mwezi uliopita nchini Afrika
Kusini.
Mgombea huyo atachuana na mgombea wa Chadema, Grace Tengega.
Jana, Mbowe alisema ingawa Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM,
alitakiwa kufahamu kwamba ni kiongozi wa nchi na ni Amiri Jeshi Mkuu
ambaye vikosi vya Ulinzi na Usalama vipo chini yake.
“Anapotoa
kauli nzito kama hiyo, inatakiwa afahamu kwamba yeye si Mwenyekiti wa
CCM tu, bali ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, hakustahili kutoa kauli kama
hiyo inayoweza kuamsha hisia,” alisema Mbowe.
Alisema kauli zake za kiitikadi za kupendelea chama chake
wakati akifahamu kuwa yeye ni kiongozi wa Watanzania wote, zinawafanya
wananchi wagawanyike kwa misingi ya vyama.
“Rais Kikwete anadai kwamba mtu wao alimwagiwa tindikali na
mwingine kutolewa macho kwa bisibisi, lakini hazungumzii viongozi na
wanachama wa Chadema waliouawa kwa kupigwa risasi na wengine kwa mabomu.
Anasema hayo huku akifahamu fika kwamba kuna vyombo vya dola na
Mahakama ambavyo vinashughulikia matukio hayo.”
February 18, 2014
Mbatia, Mbowe Wageuka Mbogo kuhusu Kauli ya Rais Kikwete..!!
11:31:00
SIASA