Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema jana alinusurika kukamatwa na makachero wa Jeshi la Polisi ili kuhojiwa kutokana na ujumbe wake aliouposti kwenye mtandao wa kijamii akiandika: “Rais Kikwete mbona umeamua kuliangamiza taifa.”
Akizungumza na gazeti la Mwananchi jana akiwa njiani
kuelekea Dodoma kushiriki Kikao cha Bunge la Katiba, Lema alisema
maafisa wawili wa polisi walimfuata katika hoteli aliyofikia Dar es
Salaam kwa lengo la kumkamata na kumpeleka makao makuu ya polisi.
Lema alisema maafisa hao, ambao walikuwa wanatumia
gari dogo, baada ya kufika hotelini hapo, waliomba aitwe na aliposhuka
walimtaka kuandamana nao, hadi makao makuu ya polisi kwa mahojiano.
“Niliwauliza nikaandike maelezo juu ya nini,
walijibu kifupi wao ni chombo cha dola na walisema wametumwa na viongozi
wa juu wa polisi na hawakuwa tayari kutaja tuhuma zangu,” alisema Lema.
Alisema baada ya polisi hao kusisitiza kutaka
kumchukua, aliwaomba aende chumbani kujiandaa kabla ya kuwasiliana na
viongozi wa chama chake na familia yake.
“Niliposhuka chini sikuwakuta na ndipo
nikashauriana na viongozi wa chama hicho na kuamua kuondoka jana mchana
Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Hata hivyo, alisema Chadema leo wanatarajia kutoa
tamko juu ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wanachama wa CCM
kuondoa unyonge dhidi ya wapinzani hasa pale wanapodaiwa kupigwa.
Mwananchi:
Mwananchi: