Lulu amemwambia paparazi wetu kuwa alishaanza kuyasahau matatizo hayo lakini hataweza kupingana na amri ya mahakama iliyopanga kuanza kusikiliza kesi hiyo kuanzia Februari 17, mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzaniajijini Dar.
“Lazima kesi iendelee na sheria ichukue mkondo wake, pamoja na kwamba nimekaa uraiani kwa kipindi kirefu na kuanza kusahau mambo hayo,” alisema Lulu.
Alipoulizwa anachokitegemea katika kesi hiyo, msanii huyo alidai kwamba hana cha kukitegemea zaidi ya kukesha akimuomba Mungu.
“Nakesha nikiomba, namwamini Mungu atanisaidia kama alivyosikia kilio changu cha kuomba dhamana,”aliongeza.
Msanii huyo anakabiliwa na kesi ya kumuua bila ya kukusudia aliyepata kuwa msanii nguli katika tasnia ya filamu za Kibongo, Kanumba Aprili 7, mwaka 2012.
Aidha, baada ya kuachana na Lulu, Ijumaa lilizungumza namama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa juu ya kutajwa kwa kesi hiyo na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo;
Ijumaa: Unajisikiaje kuona Lulu akipandishwa kizimbani tena?
Mama Kanumba: Mmmh! Kwa kweli najisikia vibaya sana jamani.
Ijumaa: Unajisikia vibaya kwa kuwa Lulu anapandishwa kizimbani au...?
Mama Kanumba: Pamoja na hilo lakini kesi hii inanikumbusha machungu ya mwanangu, naona mambo ndiyo yamefufuka upya wakati nilishaanza kuyasahau.
Ijumaa: Unasemaje kuhusu kushtakiwa kwa Lulu?
Mama Kanumba: Binafsi sijamshitaki Lulu ni serikali ndiyo iliyofanya hivyo, tuache sheria ichukue mkondo wake.