MBUNGE wa Bahi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omar Baduel amesema hatajiuzulu kwenye nafasi hiyo, kutokana na kuandamwa na baadhi ya madiwani kwa tuhuma za kutumia vibaya fedha za mfuko wa jimbo. Alitoa kauli hiyo juzi kwenye kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya Bahi.
Alisema hayo baada ya kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yake, kutoa taarifa na kuonesha Mbunge huyo alitumia kwa maslahi yake fedha za Mfuko wa Jimbo, ambao hutolewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
“Sio kweli hayo yaliyoandikwa kwenye taarifa, niliitwa kwenye tume, niliyosema humo hayamo, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,” alisema.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kuandamwa na baraza hilo la madiwani, kwani hata alipokuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, ilikuwa hivyo, hali iliyosababisha ajiuzulu nafasi hiyo, lakini alipoamua kugombea Ubunge alipata.
“Hamnitendei haki, nimesikitishwa na taarifa hiyo yenye nia ya kufanya nitoke kwenye ubunge, ila namshukuru Mwenyezi Mungu sina sauti ninaposhambuliwa na kundi la watu,” alisema Mbunge huyo. Alisema hawezi kubadilisha makusudio na nia ya watu, ambao wamekuwa wakimuandama mara kwa mara.
“Safari hii sijiuzulu, kuna watu wanaota Ubunge humu,” alisema.
Akisoma taarifa ya tume hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhakiki Fedha za Mfuko wa Jimbo,Julius Chitojo alisema baraza la madiwani lililoketi Oktoba 31, mwaka jana, lilipokea hoja binafsi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Mfuko wa Jimbo.
Alisema baraza liliazimia kuunda kamati ya watu wanne ili kufuatilia na kubaini ukweli wa hoja, zilizotolewa na Diwani wa Lamaiti, Donald Mejitii kuwa mbunge huyo alifanya ubadhirifu wa fedha zilizotolewa kwa vikundi, ununuzi na usambazaji wa majembe ya kukokotwa na ng’ombe hasa katika kipindi cha kuanzia Agosti mwaka jana.
Pia alisema michango ya fedha za wananchi wa kijiji cha Chibelela kwa ajili ya kusafisha kisima cha maji zilichukuliwa na mbunge huyo, lakini hazikutumika kwa kazi iliyopangwa.
Mwenyekiti huyo alisema kikao cha kamati ya maendeleo ya Mfuko wa Jimbo, kilichofanyika Aprili 30, mwaka jana kiliidhinisha Sh milioni 17 kwa ajili ya ununuzi wa majembe 117 na Sh milioni 3.2 kwa ajili ya usafirishaji wa majembe hadi kwa walengwa.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia Oktoba 30, mwaka jana, majembe yaliyosambazwa yalikuwa ni 85 yenye thamani ya Sh milioni 14.5, kati ya hayo majembe 78 yaliuzwa kwa Sh 110,000 kila moja sawa na Sh milioni 8.5.
Taarifa hiyo ilisema fedha nyingine za uuzaji wa majembe hayo, zilikuwa zikikusanywa na Msaidizi wa Mbunge huyo, Saidi Kayumbo ambaye baada ya kuhojiwa na kamati, alisema fedha hizo alikuwa akipeleka kwa mbunge huyo, badala ya fedha hizo kupelekwa halmashauri.
Pia, mbunge huyo alikuwa akivitaka vikundi kutumia akaunti ya Jumuiya ya Akiba na Maendeleo Bahi (BASATA) ili fedha zao za maendeleo ya ziingie humo, licha ya kuwa vikundi husika, vilikuwa na akaunti za benki.
Alisema kutokana na kubaini hayo, baraza lichukue hatua stahiki kwa mbunge huyo pamoja na kurejesha fedha zote alizochukua, ambazo zilitengwa kwa shughuli za maendeleo.
Diwani wa Lamaiti, Donald Mejitii alidai mbunge huyo alikuwa akitumia gari lake kusambaza pembejeo hizo huku akiwadai wananchi fedha za usafiri.