Ujira wa usaliti ni aibu kubwa! Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Baba Anorld almaarufu Ngosha, amedai kumfumania laivu mkewe, Anjela ‘Mama Anorld’ akiwa chumbani na shemeji yake aliyetajwa kwa jina moja la Paulo.
Fumanizi hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii, nyumbani kwa wanandoa hao huko Vingunguti-Mikoroshoni, Dar baada ya Ngosha kumwekea mkewe huyo mtego.
Ilielezwa kuwa awali, Ngosha alikuwa akishirikiana na Paulokwa mambo mengi na hakuwa na shaka naye lakini kuna siku moja majirani walimwambia ‘Oyaaa…babu shtuka mali zako zinaliwa, tena kikulacho ki nguoni mwako’.
Ilielezwa kuwa baada ya kuambiwa maneno hayo alitafakari lakini akashindwa kupata majibu hadi pale alipotamkiwa kabisa kuwa jamaa yake anamsaliti kwa mkewe.
Ngosha alisema katika uchunguzi wake, wapambe walimng’ata sikio kuwa anazungukwa na Paulo ambaye amekuwa akimuita mama Anord shemeji huku akimng’ong’a Ngosha kisogoni.
Ilisemekana kuwa wapambe hao walimtonya Ngosha kuwa akiwa hayupo mgoni huyo na mkewe huingia chumbani kwake na kufanya yao.
MTEGO WATEGWA, OFM MZIGONI
Habari zilieleza kuwa baada ya ‘kujazwa sumu’ juu ya taarifa hizo, Ngosha aliwaomba wapambe hao wamsaidie kutega mtego huku Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya GlobalPublishers ikiomba kuingia mzigoni.
ILIKUWAJE?
Ngosha aliambiwa ajifanye amesafiri na kutarajia kurudi kesho yake.
Akiwa kazini, alimpigia simu mkewe akamtaarifu kwamba asimuandalie chakula kwa kuwa kuna ‘kijisafari’ cha dharura na kutarajia kurudi kesho yake.
Ngosha hakusafiri, badala yake alikuwa mtaa wa pili huku mashushushu wake wakilizunguka eneo la tukio na kuangalia kila kilichokuwa kikiendelea kisha kutoa taarifa kwake.
PAULO AWASILI KWA MBWEMBWE
Ilipofika saa 3:43 usiku, Paulo aliwasili eneo la tukio na kuingia chumbani kwa Ngosha akiwa na kifurushi chenye chipsi na vipapatio vya kuku.
Bila kujua nje kuna wapigachabo waliopandikizwa na Ngosha, wawili hao walianza kupiga stori za ‘Kivalentine’s Day’ wakijua mwenye ndoa yake alikuwa safarini.
‘TAP’ TAA YAZIMWA
Kwa mujibu wa wapigachabo hao, saa 6:12 usiku, yale mazungumzo yalikatika ambapo wawili hao walizima taa ndipo mashushushu walipomtaarifu Ngosha.
NGOSHA ARUKIA MLANGO
Saa 6:14 usiku, Ngosha alipokea simu kutoka kwa wapigachabo wake waliomtaarifu kuwa tayari mambo ‘yamekwiva’ chumbani kwake na ndipo mwenye mali huyo alipokimbilia eno la tukio.
Alipofika aliurukia ‘samasoti’ mlango wa mninga ambao ulimdindia na kukataa kuvunjika.
Ngosha, akiwa kwenye tafakuri kuntu ya namna ya kuvunja mlango, baba mwenye nyumba aliyejitambulisha kwa jina moja la Ndosi alitokea na kumdhibiti huku akimsihi asifanye vurugu wala kuua mtu bali ajaribu kuwagongea kiustaarabu ili kuunusuru mlango wake.
WAVAA CHAPUCHAPU
Saa 6:21 usiku, wakati wakigongewa walitumia nafasi hiyo kuvaa chapuchapu na kufungua mlango wenyewe ambapo liliibuka varangati zito kati ya wawili hao walionaswa na Ngosha na kundi lake ambapo palichimbika.
Kitendo cha kumfumania mkewe laivu kilimfanya Ngosha amwage chozi la kiutu umzima kutokana na kutoamini alichokishuhudia.
MGONI APIGWA FAINI
Saa 6:45 usiku, ingawa varangati lilikuwa kubwa lakini wasamaria wema waliingilia kati na kuwatuliza kisha kuwataka Ngosha na mgoni wake (Paulo) wakae kitako na kuyazungumza kiutu uzima kwa maana hata Rich Mavoco ameimba kwenye Wimbo wa Roho Yangu kuwa ‘ku….. ni siriya ndani’ hivyo nao walifanye jambo hilo liwe siri.
Paulo na Angela waliwekwa kitako na wasamaria wema pamoja na mwenye mke na kujadiliana jinsi ya kufanya ambapo awali Paulo alisema atampa Ngosha faini ya Sh. milioni moja ili yaishe.
Wakati Ngosha akijiandaa kupokea kitita chake, alishangaa Paulo alipomuambia fedha hiyo waandikishiane kimaandishi kwa kuwa hakuwa nayo mkononi.
Ngosha aliona longolongo na kuomba msaada wa wasamaria wema wamsaidie kuwafikisha watuhumiwa wake polisi.
WAGONI WAPELEKWA POLISI MSOBEMSOBE
Mishale ya saa 7:42 usiku, wagoni hao walitembezwa mtaani wakipelekwa kituo cha polisi ambapo ilipofikia saa 8:34 usiku, walikuwa wamefikishwa Kituo Kidogo cha Polisi cha Buguruni Kwamnyamani, Dar.
Wakiwa kituoni hapo, baba mwenye nyumba wao alitoa lake la moyoni na kuwakabidhi wote waliofumaniana kituoni hapo na kujivua lawama.
Hata hivyo, hadi OFM inaondoka kituoni hapo, bado wahusika walikuwa wakihojiwa ili sheria ichukue mkondo wake.