Pages

February 16, 2014

Kigogo wa CCM Ataja Siri Mpya ya Wauzaji Dawa za Kulevya.

MBUNGE wa Kigamboni, Faustine Ndungulile ameanika siri na aina mpya ya wauzaji wa dawa za kulevya wanayoitumia katika kupanua wigo wa watumiaji wa madawa ya kulevya Duniani kupitia watoto wadogo. Ndungulile aliyasema hayo wakati akifungua Baraza la Vijana la Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia wilaya ya Temeke uliofanyika katika ukumbi wa Malaika, ambapo alibainisha bayana wauzaji wa madawa ya kulevya wamekuja na mtindo mpya wa kuwafundisha watoto wadogo kutumia madawa ya kulevya kupitia kwenye vyakula wanavyopewa wakiwa shuleni pamoja na kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba taratibu huanza kujifunza kutumia dawa za kulevya na hata siku za usoni inawawia vigumu kuacha matumizi ya dawa hizo.
“Wauzaji wa madawa ya kulevya ni watu hatari sana kwani siku hizi wameanzisha mtindo wa kuwachanganyia watoto wadogo kwenye vyakula pamoja na kuyapaka madawa hayo ya kulevya kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba huanza kujifunza matumizi ya madawa ya kulevya tangu wakiwa watoto na ni ngumu kuchomoka katika mtego wa matumizi ya madawa hayo katika maisha yao”, alisema Ndugulile.
Kama haitoshi Ndungulile alianika bayana matatizo makubwa yanayowasibu vijana kwa sasa kuwa ni madawa ya kulevya pamoja na maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo alibainisha waziwazi kuwa nguvu kazi ya taifa la leo imekuwa rehani kupitia mitego hiyo. Mbunge huyo wa Kigamboni ambaye kitaaluma ni Daktari aliweka waziwazi kuwa licha ya takwimu za kushuka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi kushuka kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5.1 bado tatizo ni kubwa kupita maelezo kwa vijana nchini.
sembe
“Kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao ambao ni asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika kwa upande wa vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya, mmojawao ambaye ni asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali ni mbaya sana kwa vijana.” Alisema Ndungulile.
Mbunge huyo wa Kigamboni aliwaasa wajumbe hao wa Baraza la UVCCM (W) Temeke na vijana wote nchini kuwa mbali na matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake wajibiidishe zaidi katika kufanya mambo yenye faida kwao kupitia shughuli za kiuchumi kwa kuchangamkia fursa zilizopo.
 Mjumbe wa Baraza la UVCCM, Ndugu Emmanuel John akichukua karatasi ya kupigia kura.
Wakati huo huo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya Temeke wamefanya uchaguzi wa majimbo yaliyopo ndani ya Wilaya hiyo na kupata Wenyeviti na Makatibu wapya wa majimbo. Baraza hilo la Vijana ambalo lilifunguliwa na Mgeni rasmi Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndungulile ambaye wakati wa ufunguzi aliwaasa vijana kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya na kujikinga zaidi na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani hali iliyopo inatisha sana kwa vijana.
“Kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao ambao ni asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika kwa upande wa vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya, mmojawao ambaye ni asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali ni mbaya sana kwa vijana.” Alisema Ndungulile.
Ndugu Ndungulile ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Temeke aliwaasa na kuwatia moyo vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa  na uchaguzi mkuu hapo mwakani naye kwa nguvu zake zote atapambana katika kuwatetea vijana wenye sifa stahiki kwani anaamini vijana ni nguvu kazi ya sasa ya Taifa.
Ndugu Ndugulile aliwaasa na kuwatakia uchaguzi mwema wajumbe wa Baraza hao wachague viongozi wenye sifa wanaowataka kwani yeye kama Ndugulile ameanika wazi kuwa hajashiriki kupanga safu za viongozi badala yake jukumu hilo limeangukia mikononi mwa wajumbe.
Kwenye baraza hilo la Vijana ambalo lilikuwa ni baraza la kazi wamechagua viongozi wa majimbo ya Kigamboni na Temeke yanayopatikana ndani ya Wilaya ya Temeke. Kwa upande wa Temeke waliojitokeza kuomba nafasi ya Uenyekiti ni Arnord Sangawe aliyepata kura 48, Julius Mkada aliyepata kura 24 na Peter Sillo aliyepata kura 4. Mshindi wa nafasi ya Uenyekiti wa Jimbo la Temeke UVCCM ulinyakuliwa na Arnord Sangawe. Waliojitokeza kwenye nafasi ya Ukatibu walikuwa ni Athumani Nyamlani aliyepata kura 6, Juma Ndwangila aliyepata kura 59 pamoja na Laurence Limwata aliyeapata kura 11. Hivyo nafasi ya Ukatibu kuchukuliwa na Juma Ndwangila.
Kwa upande wa jimbo la Kigamboni wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa jimbo walikuwa ni Ally Makwilo aliyepata kura 28, Shaaban Mbegu aliyepata kura 7 na Yasin Kanyama aliyepata kura 43. Hivyo Yasin Kanyama akatangazwa ndiye mshindi wa Uenyekiti wa Jimbo la Kigamboni kupitia UVCCM.
Halikadhalika upande wa makatibu wagombea wa jimbo la Kigamboni walikuwa ni Kambarage Makongoro aliyepata kura 27, Mustaffa Pilla aliyepata kura 32 na Salum mpili aliyepata kura 16 na matokeo hayo yalimpa ushindi Ndugu Mustafa Pilla kuwa ndiye Katibu wa jimbo la Kigamboni kupitia UVCCM.