WANAFUNZI wa chuo cha ualimu Kleruu kilichopo Gangilonga mjini Iringa, wamefanya maandamano wakipinga kukosa huduma ya umeme kwa wiki ya tatu sasa baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia.
Maandamano hayo yaliyoanzia chuoni hapo leo kuelekea ofisini na hatimaye nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, yalidhibitiwa na Jeshi la Polisi yakiwa yamekaribi shule ya msingi Um-salam kwa kile kilichoelezwa kwamba hayakuwa na kibali..
Rais wa serikali ya wanafunzi ya chuo hicho, Manfred Joachim alisema wametii amri ya Polisi lakini watayafanya tena Jumatatu baada ya kukamilisha taratibu zote ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha Polisi.
Joachim alisema wameamua kutumia mbinu hiyo ili kuongeza msukomo kwa uongozi wa chuo na serikali kuitatua kero hiyo.
“Hatuwezi tena kujisomea usiku na mafunzo ya teknlojia ya habari na mawasiliani yaani ICT yamesimama; wanafunzi wamekata tamaa, hawajui hatma yao wakati ada wamelipa,” alisema.
Wakiwa wamekusanyika katika uwanja wa michezo wa chuo hicho chini ya ulinzi wa Polisi, kiongozi huyo alisema huduma ya maji nayo ni kero kubwa chuoni hapo.
“Wakati mwingine zinaweza kupita zaidi ya siku mbili hatujaoga; yote hayo ni kwasababu tuaambiwa na uongozi wa chuo kwamba hawana fedha za kulipia huduma hizo,” alisema.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Anjelist Mlenga alisema uongozi wa chuo unawaonea huruma wanafunzi hao lakini akakosoa taratibu wanazozitumia kudai huduma hizo.
Akiwa hajui kiasi cha fedha kinachodaiwa kwa ajili ya huduma ya maji, Mlenga alisema deni la umeme chuoni hapo ni zaidi ya Sh Milioni 2.5.
Alisema Mkuu wa chuo hicho amekwenda wizarani kufuatilia fedha hizo kwakuwa wao ndio wenye jukumu la kulipia huduma hizo.
“Mkuu wa Chuo yupo wizarani, naomba muwe wavumilivu kwani hata kama atakubaliwa fedha hizo, kwa taratibu za serikali inaweza kuchukua wiki nyingine kuzipata,” alisema.
Akizungumzia ombi la wanafunzi hao la kukifunga chuo hicho mpaka pale huduma hizo zitakaporejea, Mlenga alisema “ ni jambo linalojadirika, tutaona mpaka wiki ijayo hali itakavyokuwa na tutaangalia cha kufanya.”
Aliwasihi wanafunzi hao kuacha kuyachanga madai yao na itikadi zao za kisiasa kwa kuzingatia kwamba mambo hayo yanapigwa marufuku katika taasisi za elimu.