BUNGE Maalumu la Katiba, limeanza
chini ya mfumo wa kidijitali ambao pamoja na masuala mengine, vipaza
sauti vyote viko chini ya udhibiti wa Mwenyekiti hali ambayo haitaruhusu
mbunge kuvitumia bila ridhaa ya kiti.
Hayo yalifahamika jana bungeni mjini
hapa, wakati Sekretarieti ikitoa maelekezo kwa wajumbe kuhusu ukaaji na
jiografia ya ukumbi.
Aidha wajumbe wamehakikishiwa kuwepo
usalama wa kutosha huku wakiambiwa wakubaliane na upekuzi wa hali ya juu
unaofanyika kutokana na mazingira ya sasa ambayo suala la usalama ni
tata.
Chini ya usimamizi wa Katibu wa Bunge, Dk
Thomas Kashililah na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis
Hamad, ilielezwa, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu sasa anao uwezo wa kuzima
kipazasauti za mjumbe akiwa mezani kwake.
“Sauti ya kaa chini ikisikika, ukitaka
kuendelea kuzungumza, sauti haitasikika,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa
Teknolojia ya Habari (IT), Didas Wambura.
Kutokana na mfumo huo, kipaza sauti cha kwanza kikishawashwa, kinaonesha rangi nyekundu.
Wengine wakiwasha, wanaoneshwa rangi
ya kijani kuashiria kwamba wasubiri. Viashiria hivyo vinakuwa kwenye
kiti ambaye anavitumia kuruhusu wazungumzaji.
Mfumo utaweza? Hata hivyo muda mfupi
baada ya wataalamu kuwasilisha maelekezo, walipopewa muda wa kuuliza
maswali au kupata ufafanuzi, walijitokeza wajumbe wengi waliotaka
kuzungumza ambao baadhi, baada ya kudhibitiwa na mfumo, walipaza sauti
bila kutumia vipaza sauti wakitaka wapewe nafasi.
Wakati huo huo Wambura alisema kila
mjumbe ana kadi inayomwezesha siyo tu kufungulia mlango, bali kutumia
katika kuzungumza kupitia vipaza sauti hivyo na pia inamwezesha kupiga
kura.
Kaimu Mkuu wa Usalama wa Bunge, Peter Magati alisema wameongeza vituo vya upekuzi na akaomba wajumbe wakubaliane na hali hiyo.
“Mazingira ya sasa hivi ya hali tata ya usalama ndiyo sababu ya upekuzi wa namna hii,” alisema.
Aliendelea kusema, “tumejiandaa
kuhakikisha mnakaa kwa amani na utulivu ndani na nje ya Bunge.” Kuhusu
wageni, alisema watakuja kwa taarifa na akataka wajumbe kuhakikisha
wageni wao wanakuwa katika mavazi ya staha yasiyo na walakini. Masuala
mengine waliyohakikishiwa wajumbe, ni umeme kutokatika.
Sanjari na hilo, Mkuu wa Wakala wa
Serikali Mtandao, Dk Jabir Bakar alisema pia ipo Wavuti ya Bunge Maalumu
itakayokuwa ikirusha shughuli zote za Bunge moja kwa moja sanjari na
Televisheni ya Taifa (TBC).
Huduma za matibabu zinapatikana katika
hospitali iliyoko bungeni na ikitokea matibabu yakashindikana, mjumbe
anaruhusiwa kwenda hospitali nyingine ya Serikali au binafsi kwa ushauri
wa daktari na gharama za matibabu zitarudishwa.
Aidha wajumbe wamepewa orodha ya hoteli huku wakiaswa kutokwenda maeneo yanayohatarisha maisha yao.
Posho Taarifa ya Mhasibu Mkuu wa Bunge
ilieleza kwamba licha ya wajumbe kulipwa posho ya kujikimu kila siku
huku posho maalumu ikilipwa kwa wiki, vile vile wenye wasaidizi
watalipwa posho ya kujikimu.
Malipo mengine wanayopewa wajumbe ni
gharama za usafiri ambazo zitarejeshwa baada ya mhusika kuwasilisha
tiketi ya usafiri aliotumia. Pia upo utaratibu wa kurudisha mafuta kwa
waliotumia usafiri binafsi.
Wajumbe wenye watoto wachanga
wameambiwa wawasiliane na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kwa
ajili ya kupewa utaratibu juu ya eneo la kutolea huduma.
Ukaaji ndani ya ukumbi huo wenye viti
676, umezingatia majina, wenye mahitaji maalumu hususani wenye ulemavu
na pia wenye mahitaji maalumu ya kiusalama kama vile Waziri Mkuu.
Wajumbe Baada ya maelekezo kutolewa
ukumbini, baadhi ya wajumbe walilalamikia masuala mbalimbali, wakiwemo
wenye ulemavu waliotaka mazingira rafiki kwao ikiwemo kuwepo wakalimani
kwenye televisheni.
Vile vile suala la usawa wa jinsia katika
uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu wake, lilijitokeza kutoka miongoni mwa
wajumbe. Mjumbe wa kwanza kusimama alikuwa Tundu Lissu, ambaye alitaka
ufafanuzi kutokana na kile alichosema baadhi ya nyaraka muhimu hazimo
kwenye makabrasha.
Mwingine, Mussa Ali Kombo,
alilalamikia posho akisema wapo waliofika Februari 16 mwaka huu lakini
hawakujisajili jambo ambalo limewanyima posho ya kujikimu. Alitaka
wafikiriwe kupatiwa posho hiyo.
Ernest Kimaya alitaka kufahamu iwapo
wenye ulemavu watapatiwa maandishi makubwa. Kwa upande wake, Amon Mpanju
alihoji kama kutakuwepo wakalimani wa lugha za alama ili watu walio
kundi hilo wafuatilie yanayojadiliwa kwenye Bunge.
Naye Julius Mtatiro alihoji kuhusu
stahiki za wajumbe akitaka posho maalumu wanayopewa, viwango vitajwe
waelewe. Kwa upande wake, Kangi Lugora alitaka wagawiwe mapema rasimu ya
Kanuni za Bunge hilo.
“Iko tabia ya kuuziwa mbuzi kwenye
gunia…tugawiwe haraka. Lazima tuwe na muda wa kutosha. Mpaka kieleweke
mimi sitoki bila kuwa na kanuni,” alisema.
Hata hivyo Katibu wa Bunge, Dk Kashililah
alisema suala la kanuni inabidi kusubiri apatikane Mwenyekiti wa Muda
ambaye ndiye mwenye jukumu la kuandaa kanuni. Akizungumzia usawa wa
kijinsia katika kupata Mwenyekiti na Makamu wake, Kashililah alisema
uchaguzi huo ni suala la kisheria.
“Mnatubebesha mzigo tu, naliacha kwa
mtaalamu,” aliwaambia wajumbe. Kuhusu maandishi makubwa na wakalimani
kwa wenye ulemavu, Katibu wa Bunge alisema huduma hizo zitapatikana
mkutano utakapoanza.
Aidha kuhusu hoja ya Lissu, Kashililah
alikubaliana naye na akasema nyaraka zinaendelea kuchapishwa na kabla ya
kuanza kupitia rasimu ya katiba, zitakuwa zimepatikana. Akijibu
aliyelalamikia posho, Kashililah alisema ambao hawakulipwa posho ya
kujikimu lakini walifika Dodoma Februari 16 wawasilishe uthibitisho.
Source: Habarileo