Pages

February 11, 2014

NABII ALISHWA SUMU NA KUZIDIWA KWENYE MADHABAHU

SHETANI bado anajifanya haogopi, kila kukicha anasababisha. Safari hii amemjaribu mtumishi wa Mungu, Nabii Nicolas Suguye wa Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho lililopo Kitunda-Kivule jijini Dar es Salaam ambapo yupo katika hali mbaya kufuatia kulishwa sumu na mtu asiyejulikana, Uwazi lina mkasa mzima.

Nabii Nicolas Suguye.
SIKU YA TUKIO
Taarifa zilizolifikia gazeti hili juzi kutoka kwa waumini wake zinadai kuwa tukio hilo lilijiri Februari 2, 2014 ambapo nabii huyo mwenye karama ya uponyaji alikuwa madhabahuni akihubiri neno lenye mamlaka na matendo ya miujiza lakini ghafla alijisikia maumivu ya tumbo, mwili kukosa nguvu na kichefuchefu.

ASHINDWA KUENDELEA NA HUDUMA
Kwa mujibu wa baadhi ya waumini hao, ilifika mahali mtumishi huyo wa Mungu alishindwa kuendelea na mahubiri, ikabidi atolewe na huduma yake kuchukuliwa na wasaidizi wake.

HALI YAZIDI KUWA MBAYA
“Baada ya kutolewa madhabahuni tuliamini hali itapoa baada ya kupumzika kidogo, lakini wapi? Hali yake ilizidi kuwa mbaya, sasa alikuwa hawezi kuzungumza sawasawa,” alisema muumini mmoja wa kanisa hilo.

AKIMBIZWA HOSPITALI YA AMI
Habari zaidi zinasema kuwa, ilipoonekana mtumishi huyo hapati nafuu, mkewe, Anna Suguye kwa ushirikiano na waumini wengine walichukua gari na kumkimbiza Hospitali ya African Medical Investment (AMI) iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako alilazwa kwa matibabu ya awali. Ikumbukwe kuwa hata Askofu Moses Kulola alifia kwenye hospitali hiyohiyo.

WAUMINI WABUBUJIKWA MACHOZI
Wakati mchungaji huyo anapelekwa hospitalini, baadhi ya waumini walikuwa wakibubujikwa machozi kwa vile  walikuwa hawajui hatima ya kiongozi wao huyo.

UWAZI LATINGA KANISANI
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, Jumamosi iliyopita Uwazi lilitia timu kanisani kwa nabii huyo.
Ilikuwa vigumu kumpata kwani baadhi ya watumishi walidai hayuko katika afya ya kuonana na watu baada ya kutoka hospitalini.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye mtumishi huyo wa Mungu aliwasili akiwa na mke wake. Alionekana amedhoofu pia hana raha.
ALIFUNGUKIA UWAZI
Baada ya salamu, Uwazi lilijitambulisha kwa mtumishi huyo na kumpa pole kwa yaliyomkuta ambapo alisema:

“Kwanza namshukuru Mungu wangu amenipigania hadi leo hii naongea nanyi. Kwa mujibu wa daktari nililishwa sumu kali sana japokuwa hakuniambia ni aina gani. Ila aliniahidi majibu kamili nitayapata baadaye leo.”
ILIKUWAJE?
“Nakumbuka ilikuwa Januari 28, mwaka huu ndipo nilianza kupata maumivu makali. Nilikuwa nikiendelea na ibada kanisani wiki nzima huku nikipata maumivu.

“Hata hivyo, nilikuwa nasali bila kujua ni kitu gani kilikuwa kikinisumbua kwenye mwili wangu. Nilifikiri ni ugonjwa wa kawaida ambao ningeweza kupata nafuu haraka lakini haikuwa hivyo.
KILICHOMKABILI
Nabii Suguye aliendelea kusema kuwa kikubwa kilichokuwa kikimsumbua kwa wakati huo ni kutapika huku mwili ukifa ganzi ndipo siku ya ibada akazidiwa na kukimbizwa hospitali.

“Pia daktari aligundua presha yangu ilishuka sana, nilitundikiwa dripu ya maji na kuchomwa sindano ya kupunguza maumivu.
“Hata hivyo haikusaidia, ikabidi wanichome sindano nyingine na kuchukua vipimo vya damu na picha ya X-ray, hawakubaini kitu. Halafu pia nikawa sipati choo, nikijisaidia inatoka damu.
SUMU YA MUDA MREFU
“Vipimo walivyochukua baadaye walibaini sumu niliyolishwa ilikuwa ya muda mrefu, tena ni Mungu bado ananipenda kwani sumu hiyo daktari alisema ni kali na nisingeweza kuchukua muda mrefu nikiwa hai,” alisema Suguye.

AWATUHUMU WABAYA WAKE
Akizungumzia hisia zake juu ya nani yuko nyuma ya sumu hiyo, Nabii Suguye alisema:
“Huenda wakawa wapinzani wangu wa huduma ya Mungu lakini kumjua ni nani, ilikuwa wapi na lini nilipewa si rahisi.”

HATAKI KUONANA NA MTU BAADA YA UWAZI
Suguye alisema baada ya mazungumzo na gazeti hili asingependa kuonana na mgeni mwingine yeyote kwa sababu bado hajapona sawasawa.

MAARUFU WALIOWAHI KULISHWA SUMU
Baadhi ya watu wenye majina makubwa waliowahi kulishwa sumu na kunusurika kifo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (hakutaja hospitali), msanii wa filamu za Bongo, Illuminata Poshi ‘Dotnata’ (alikimbizwa Lugalo) na aliyewahi kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Charles Kenyela (alikimbizwa TMJ). Wote hawakukumbuka siku ya kukutwa na tukio.

UWAZI HADI HOSPTALI YA AMI
Juzi, Uwazi lilifika Hospitali ya Ami na kuulizia undani wa sumu aliyolishwa Nabii Suguye lakini daktari aliyekuwa zamu alisema hana kibali cha mtumishi huyo wa Mungu cha kutoa siri ya ugonjwa wake.

NABII ARUDIWA
Baada ya kutoka Ami, Uwazi lilimpigia nabii huyo na kumuuliza kama alishapata majibu ya daktari.
“Nilikwenda, wamesema naendelea vizuri. Walinipa dawa za aina mbili tofauti. Kuhusu sumu waliniambia ilibainika kwenye haja kubwa na ilikuwa kali sana,” alisema Suguye.