Ni miaka takribani saba sasa tangu Kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba wa kampuni hewa ya Richmond iliyotumiwa kuliibia taifa na Waziri mkuu wa wakati huo Edward Lowasa ilipokutwa "Jinai"

Baada ya kubaini wizi mkubwa ulioongozwa na Edward Lowasa akiwa Waziri Mkuu na yule waziri wa nishati na madini mr Msabaha, Kamati teule ya Bunge ilitoa maadhimio/mapendekezo 16, lakini serikali imeshindwa kutekeleza mapendekezo hayo,

Swali ni, Kwanini serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kutekeleza mapendekezo hayo?


Hebu Tujikumbushe maadhimio ya Kamati ya Mwakyembe!





Mapendekezo ya Kamati Teule Mheshimiwa Spika,

Kutokana na uchunguzi wa kina tuliuainisha katika taarifa hii, Kamati Teule imejiridhisha na hivyo inatamka bayana mbele ya Bunge Tukufu kuwa mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa MW 100, uliopelekea Richmond Development Company LLC kuteuliwa na hivyo kusaini mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 23 Juni 2006 na baadaye kurithiwa na Dowans Holdings S.A tarehe 23 Desemba 2006, uligubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi na hivyo kujenga kiwingu cha mashaka ya upendeleo, ubadhirifu na rushwa ambavyo vimechangia kumuongezea mwananchi mzigo wa gharama za umeme. Aidha, Kamati Teule imethibitisha bila ya shaka lolote kuwa uteuzi wa Kampuni dhaifu kifedha, kiufundi na kiuzoefu na ambayo haina usajili Marekani wala Tanzania kama kampuni yenye ukomo wa hisa, yaani Richmond Development Company LLC, ulitokana na kubebwa bila woga wala aibu na viongozi waandamizi wa Serikali. Kutokana na msingi huo Kamati Teule inapendekeza yafuatayo:

(1) Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 (Public Procurement Act, 2004) haina nguvu ya kutosha ya kuiwezesha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kwamba Ununuzi wa Umma unaboreshwa kwa kuongeza ushindani wa ukweli na uwazi na hivyo kuipa Serikali thamani halisi ya pesa zake. Kamati Teule inapendekeza kwamba sheria hii ipitiwe upya ili kuiboresha kwa kuipa Mamlaka nguvu zaidi za udhibiti na uwezo wa kuchukua hatua pale Sheria na Kanuni zinapokiukwa, badala ya kutoa ushauri tu kama ilivyo sasa.

(2) Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma isiwajibike Wizara ya Fedha ambayo nayo ni taasisi ya ununuzi (procurement entity) badala yake iwe chombo huru kinachowajibika Ofisi ya Rais na taarifa zake kuwasilishwa Bungeni.

(3) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A, kama ilivyo mikataba kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals inatoa unafuu usiostahili kwa makampuni hayo ya umeme na kuiumiza TANESCO na hatimaye watumiaji na walipa kodi kimapato, k.m mikataba hiyo kuwa na vipengele vya kuibana TANESCO kuyalipia makampuni hayo kodi zinazohusika na uendeshaji (operations), matengenezo/marekebisho ya mara kwa mara ya mitambo (maintenance) gharama za bima, ada za mawakili na washauri elekezi (consultants) gharama za mafuta na gesi ya kuendeshea mitambo, gharama za ukodishaji mitambo (capacity charges) ambazo TANESCO hulipa kila mwezi si chini ya wastani wa shilingi bilioni 2 kwa kila kampuni, izalishe au isizalishe umeme. Kamati Teule inatoa rai kwa Serikali kuwa mikataba yote hii ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo mikataba ya madini inavyopitiwa upya sasa na Serikali. Bila kufanya hivyo, mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi na kushindwa kufikia azma ya Serikali ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

(4) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC ulikuwa wa uzalishaji umeme wa dharura kipindi ambacho nchi ilikuwa katika hali ngumu ya ukame uliokausha mabwawa yote ya kuzalishia umeme. Kamati Teule inaitaka Serikali kutathmini upya uhalali wa kuwepo na kuendelea kuwepo na mkataba huo kutokana na udanganyifu bayana uliofanywa na Richmond Development Company LLC kuhusu uwezo wake kifedha, kiufundi, na uzoefu wake katika masuala ya uzalishaji umeme; usajili na uwepo wake kisheria kama kampuni halali yenye ukomo wa hisa nchini Marekani na Tanzania; uhusiano wake kisheria na Kampuni kubwa ya Kimataifa ya Pratt & Whitney na utambulisho wa Mzungu mmoja kwa jina la John Perun kama mwakilishi wa Pratt & Whitney, mambo ambayo Kampuni hiyo kubwa ya Kimataifa imeyakanusha vikali.

(5) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu mkubwa wa kitaalamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au ukosefu wa umakini ama ubinafsi katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano, kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni za Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi wa awali (due deligence) au ukaguzi baada ya uteuzi (post qualification); kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement na proprietary information agreement; kushindwa kuona dosari kisheria za proprietary information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria kati ya Richmond Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki wa Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia kwa kubadilisha badilisha (interchangerbly) kwa makusudi; kushindwa kuwashauri Wajumbe wa GNT kwamba business card si mbadala wa hati mahsusi kisheria; kushindwa kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano kati ya Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) na Richmond Development Company LLC ambao ulizingatia baadhi ya maslahi ya nchi, uwe sehemu ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo wazi ya kuvunja Mkataba baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa kutekeleza sehemu yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao muhimu vya majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye katika majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa kilichokuwa kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake katika GNT haukuwa na tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya nchi kwa kuchangia kuiingiza nchi katika mkataba wa aibu.


(6) Katika mikataba yote na makampuni ya nje Serikali ihakikishe kuwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inatumika kikamilifu katika kupata taarifa kamili za kampuni hizo, kama vile wanahisa, mitaji na anwani. Aidha, Ofisi zetu za Ubalozi zilizo sehemu mbalimbali duniani zihusishwe katika majadiliano na makampuni yanayotoka nje ya nchi kwa lengo la kupata taarifa zao za msingi na kuboresha nguvu ya hoja ya Serikali.

(7) Madhumuni ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC yalikuwa kuzalisha umeme wa dharura kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12) tu.
Muda huo ungeweza kuongezwa baada ya kutathmini hali ya ongezeko la maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme nchini. Kabla ya muda wa tathmini hiyo haujafikiwa, wakati majadiliano yakiendelea GNT ikaongezea Richmond Development Company LLC muda wa kukodi mitambo hiyo kuwa miaka miwili (2). Kamati Teule haikuona vielelezo vyovyote vilivyojenga uhalali kwa GNT kuongeza muda huo. Uamuzi huo umeliongezea Taifa mzigo mkubwa wa gharama zisizokuwa za lazima. Mathalan, kwa upande wa capacity charges tu, TANESCO itailipa Dowans Holdings S.A jumla ya shilingi bilioni 54.8 kwa kipindi kilichongezwa cha mwaka mmoja.

Aidha, GNT ilishindwa kutambua ulaghai wa Richmond Development Company LLC kuhusu mwakilishi wa Pratt & Whitney na hivyo kuamini karatasi ambayo ilikuwa haijathibitishwa na mawakili na diskette zenye picha za mitambo ya Pratt & Whitney, vielelezo ambavyo Kamati Teule imegundua na kuthibitisha kuwa vilikuwa vya kugushi. Vilevile, bila kujali kwamba TANESCO ingelezimika kuilipa Richmond Development Company LLC shilingi milioni 152 kwa siku kama gharama ya kuweka vifaa vyao nchini, GNT ikakubali kilegelege kuitoza Richmond Development Company LLC shilingi milioni 12 tu kwa siku kama fidia kwa ucheleweshaji wa kuanza kuzalisha umeme kulingana na tarehe iliyokubalika kwenye mkataba. Kamati Teule inapendekeza kuwa Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi wa Serikali wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao kulinda maslahi ya Taifa.



(8) Pamoja na Uongozi wa TANESCO kubainisha mapungufu ya Richmond Development Company LLC na kutoa notisi tarehe 27 Octoba 2006 ya kusitisha Mkataba tena kwa ushauri mahsusi kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Mawakili, Wizara ya Nishati na Madini haikuupenda mwelekeo huo hivyo tarehe 28 Novemba 2006 baadaye Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Nazir Karamagi, Mb akiwa nje ya nchi Calgary, Canada alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Kazaura kuangalia uwezekano wa kuhaulisha Mkataba wa Richmond kwa kampuni nyingine. Siku tano baada ya mawasiliano hayo, yaani tarehe 4 Desemba 2006, TANESCO ikapokea barua kutoka Richmond Development Company LLC ikielezea nia ya kampuni hiyo kutumia haki yake chini ya kifungu 15.12 cha mkataba ili kuhamisha majukumu yake ndani ya mkataba kwenda kwa kampuni mpya ya Dowans Holdings S.A. Kamati Teule ilipata taarifa za ndani ya Wizara na TANESCO kuwa viongozi wa Wizara kama kawaida yao waliishinikiza TANESCO kuridhia ombi hilo la Richmond Development Company LLC kuhaulisha mkataba kwa Dowans Holdings S.A. TANESCO ikalazimika kuridhia uhaulishaji wa mkataba huu badala ya kutumia fursa iliyokuwepo ya kusitisha mkataba baada ya kutoa notisi ya siku thelathini. Kamati Teule inaamini kwamba uamuzi wa Wizara ya Nishati na Madini kuizuia TANESCO isitumie fursa ya kusitisha mkataba huo, unaashiria jinsi viongozi wetu wanavyojali zaidi faida na maslahi ya makampuni ya nje kuliko maslahi mapana ya Taifa. Tarehe 3 Desemba TANESCO kama ilivyoagizwa ikaridhia uhaulishwaji wa mkataba huo lakini kipindi ambacho hali ya maji katika mabwawa yetu ya kuzalishia umeme ilishaanza kurejea kuwa ya kawaida. Uamuzi huo umeingizia Taifa hasara kubwa. Hivyo basi Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Nazir Karamagi, Mb aliyeshabikia sana uhaulishaji huo, awajibishwe.



(9) Matokeo ya uchunguzi ya Kamati Teule kama yalivyoainishwa hapo juu yanadhihirisha wazi jinsi Taifa lilivyotumbukizwa kwenye hasara kubwa kutokana na mkataba huo wa Richmond Development Company LLC na Dowans Holdings S.A, kinyume na taarifa iliyotolewa na TAKUKURU (wakati huo TAKURU) kwamba Taifa halikupata hasara yoyote. Taarifa ya TAKUKURU ililenga kuficha ukweli (white wash) hivyo ikaishia kujikanganya kwa kukiri kuwepo kwa mapungufu lakini yasiyokuwa na athari. Taarifa hiyo imemong’onyoa kwa kiasi kiasi kikubwa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kilichopewa dhamana ya kupambana na rushwa na sio kuipamba ili kurejesha heshima ya umma katika taasisi hiyo. Kamati teule inapendekeza mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo.



(10) Taratibu za malipo ya madai ya mkataba wa umeme wa dharura zinafanywa kupitia Barua ya Dhamana ya Benki iliyofunguliwa kati ya TANESCO na benki ya CRDB ya dola za Kimarekani milioni 30,696,598 iliyofunguliwa tarehe 27 Desemba 2006. Kamati Teule imethibitisha kwamba hadi kufikia tarehe 19 Juni 2007 malipo yaliyolipwa na Benki Kuu yamefikia Dola za Kimarekani 35,561,598 kiasi hicho ni zaidi ya Barua ya Dhamana ya Benki kwa dola za kimarekani milioni 4,565,000 wastani wa shilingi bilioni 5.7. Kamati Teule inashangaa ni vipi Benki Kuu iidhinishe malipo hayo nje ya Barua ya Dhamana ya Benki iliyofunguliwa kati ya TANESCO, CRDB Bank na Dowans Holdings S.A. Kwa kuwa Benki Kuu ndio msimamizi mkuu wa akaunti maalum (Escrow Account), Gavana wa Benki Kuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wachunguze kwa makini uhalali wa malipo hayo na kuhakikisha kwamba udhaifu wa namna hii haujitokezi tena hapo baadaye.



(11) Wakati umefika sasa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 (Public Leadership Code of Ethics Act) ifanyiwe marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaonekana wa kawaida sasa wa viongozi waandamizi wenye dhamana kisiasa kuendelea na biashara zao wakiwa madarakani, hivyo kuwaweka kwenye mtihani mkubwa wa mgongano wa kimaslahi katika maamuzi yao. Tufike mahali ambapo sheria iwalazimu kuchagua kati ya Utumishi wa Umma au biashara binafsi. Viongozi waandamizi wenye dhamana kisiasa (mawaziri na kuendelea) kuendelea na biashara zao wakiwa madarakani hivyo kuwaweka kwenye mtihani mgumu wa mgongano wa kimaslahi.



(12) Serikali iondokane kabisa na utaratibu wa kutumia mawakala katika ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini na kuhakikisha kuwa Wizara husika ina taarifa za bei halisi ya mitambo kila wakati ili kujiepusha na mchezo wa kawaida wa mawakala kupandisha bei mara mbili au zaidi ya bei halisi. Kamati Teule ilishuhudia bei za mitambo hiyo jijini Houston, Texas Marekani kwa watengenezaji kiwandani ikiwemo kampuni ya Kawasaki Gas Turbines – Americas ambayo iko chini ikilinganishwa na bei zinazotolewa na mawakala hao, jambo ambalo lingeiwezesha Serikali kununua na kumiliki badala ya kukodi kwa muda mfupi na kwa gharama kubwa. Mathalan, MW 105 zingepatikana kwa kununua mitambo sita ya MW 17,5 kila mmoja kwa gharama ya shilingi bilioni 56.25 badala ya shilingi bilioni 108.7 tulizotandikwa na Richmond Development Company LLC mitambo hiyo ikibaki mali ya wakodishaji. Kwa kumalizia Kamati Teule ilithibitisha kwamba kauli iliyokuwa inatolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wote tuliowahoji kwamba kipindi hicho cha ukame haikuwa rahisi kupata mitambo hiyo na ilikuwa ikigombaniwa na nchi nyingi kauli hiyo ilikuwa sio ya ukweli na upotoshaji mkubwa.



(13) Utaratibu tuliourithi kutoka kwa wakoloni na kuuzoea wa kuiona mikataba ya kibiashara kuwa ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe na kuwa uwanja wa pekee wa watendaji, ambao Waziri wa Mipango Uchumi na Uwezeshaji Mhe. Dk Juma Ngasongwa (Mb) aliusifia bungeni tarehe 19 Aprili 2007 kuwa best practice wakati akijibu swali la Mhe. Masolwa C. Masolwa (Mb) Mbunge wa Bububu, umepitwa na wakati na unakiuka misingi ya demokrasia na uwajibikaji. Matokeo ya utaratibu huu ni kuwepo kwa mikataba mibovu inayoficha vipengele vinavyoibebesha Taifa mizigo mikubwa ya gharama zisizokuwa za lazima kama tulivyoainisha katika pendekezo namba 3 hapo juu. Kamati Teule inatoa wito kwa Serikali kuondokana na utaratibu huu usio na tija kwa kuzihusisha Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo. Aidha, Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa nay a muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika.



(14) Pamoja na dharura iliyokuwa inalikabili Taifa, Serikali haiwezi kuwa kinara wa uvunjaji wa taratibu, kanuni na sheria za nchi kwa makusudi. Kamati Teule imeanisha katika taarifa hii vitendo vya ubabe, ujeuri na kiburi vilivyofanywa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini alimradi kampuni waliyoitaka iteuliwe kiasi cha kupindisha hata maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote, kukaidi ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma mara tatu mfululizo na kinyume na maagizo ya Baraza la Mawaziri lililotaka Sheria ya Ununuzi wa Umma izingatiwe, kukiuka sheria kwa makusudi kwa kuingilia mchakato wa zabuni wa taasisi nyingine ya ununuzi, kuvipuuza vyombo vya ndani vya maamuzi vya TANESCO (Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Zabuni n.k), kuilazimisha Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuridhia maamuzi yaliyofanywa na Wizara ya kuibeba Richmond Development Company LLC kinyume cha sheria na taratibu n.k. Wizara hiyo katika kuibeba Richmond Development Company LLC ilifikia hatua ya kupotosha kwa makusudi ushauri wa Wizara ya Fedha uliozuia malipo ya awali ya Dola za Kimarekani Milioni 10 katika Barua ya Dhamana ya Benki ya Richmond Development company LLC. Siku iliyopotosha ilikuwa tarehe 6 Octoba 2006. Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura haujaanza.



(15) Utaratibu wa kuteua wakurugenzi na makamishna katika Wizara kuwa wajumbe wa bodi za wakurugenzi za mashirika yaliyo chini ya Wizara, unazua mgongano wa kimaslahi, kudhoofisha usimamizi na uwajibikaji, hivyo Serikali iupige marufuku mara moja. Mfano Kamishna wa Nishati ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ambaye alishiriki kwenye kikao kilichowakataa wazabuni wote kuwa hawafai na kuishauri Serikali vilivyo, aliporejea Wizarani alishiriki katika kutengua maamuzi ya Bodi ya TANESCO.



(16) Uhuru mkubwa ambao viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini waliutumia bila wasiwasi katika kuhakikisha kwamba kampuni waliyoitaka, Richmond Development Company LLC, inapewa zabuni ya umeme wa dharura; maelekezo ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu kwa Wizara katika kila hatua ya mchakato huo; upendeleo wa dhahiri ambao Richmond Development Company LLC iliupata kutoka taasisi mbalimbali za Serikali k.m Kituo cha uwekezaji (TIC) ambacho kilifikia hatua ya kufumbia macho baadhi ya taratibu zake za msingi ili kuipa kampuni tanzu ya Richmond Development Company LLC cheti cha uwekezaji haraka iwezekanavyo; kutotimiza masharti ya Bodi za Makandarasi na Wahandisi na Wizara ya Nishati na Madini kuikingia kifua kampuni hiyo isichukuliwe hatua za kisheria; uteuzi wa mwisho wa Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kufanywa na Waziri Mkuu mwenyewe tarehe 21 Juni 2006; uamuzi wa kuiteua Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kusafishwa na TAKURU ( sasa TAKUKURU) kuwa ulikuwa wa wazi na wa haki; uamuzi wa Serikali kuizuia TANESCO isivunje mkataba na kampuni hiyo licha ya sababu zote kisheria kuwepo, ni baadhi tu ya viashiria vya nguvu kubwa iliyo juu ya Wizara ya Nishati na Madini kutumika katika suala hili na Kamati Teule kutokana na ushahidi wa kimaandishi, kimazingira na wa mdomo, inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu. Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Kamati Teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa hizo zinazomgusa moja kwa moja Mhe. Waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond Development Company LLC. Hata hivyo Kamati Teule imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge letu Tukufu. Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge. Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake. Kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia Kamati Teule ya Bunge ilifadhaishwa sana na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ya kukaidi amri ya kuwasilisha nyaraka zinazohitajika na Kamati Teule.Kamati Teule inaliomba Bunge litafakari kitendo cha aina hii na kufikiria hatua za kuchukua dhidi ya watendaji wa namna hiyo.7.0


SHUKRANI

Mheshimiwa Spika, naomba kurudia kukushukuru wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwa kutupa heshima hii kubwa ya kuunda Kamati Teule ya Bunge