Mwanamziki mashuhuri wa muziki wa 'pop' kutoka Canada Justin Bieber amefunguliwa mashtaka ya kumpiga dereva wa gari la kifahari la kukodisha mwezi Disemba mwaka uliopita.
Bwana Bieber aliye na umri wa miaka 19 alikaribishwa katika katika kituo cha polisi cha Toronto na kikosi kikubwa cha wapiga picha za televisheni pamoja na unyende wa mashabiki wake chipukizi.
Amefunguliwa mashtaka chini ya juma moja baada ya kukamatwa mjini Florida marekani kwa shutuma za kuendesha gari akiwa mlevi na mashtaka mengine.
Mwanasheria wa Marekani anayemwakilisha mwimbaji huyo amesema mteja wake hana makosa.
Kwa mujibu wa polisi wa Toronto, yapata saa 02:50 saa za Canada tarehe 30 Disemba, gari la kifahari liliwasili kumchukuwa bwana Bieber na wenzake watano katika kilabu moja ya starehe ili kuwarejesha katika chumba chao cha hoteli.
Na wakati walipokuwa njiani, dereva huyo pamoja na mmoja wa abiria wake, aliyetajwa kama bwana Bieber, wanasemekana kuanza kufokeana maneno makali.
Abiria huyo "alimgonga dereva wa limousine hiyo kwenye kisogo mara kadhaa", polisi wamesema.
Dereva huyo anasemekana kusimamisha gari lake na kisha kutoka nje na kuwaita polisi. Mshukiwa 'alichana mbuga' kabla ya polisi kuwasili.
Bwana Bieber alijisalimisha kwa polisi Jumatano. Anatarajiwa kufikishwa kizimbani tarehe kumi mwezi Machi.
Howard Weitzman, wakili wa Bwana Bieber mjini California, amesema msanii huyo hana hatia na kwamba anatarajia kesi hiyo itachukuliwa kama kosa dogo tu.
Kuendesha gari akiwa mlevi
Kadhalika siku ya Jumatano, ombi la kutaka bwana Bieber atimuliwe nchini marekani lilipata sahihi laki moja.
Ombi hilo liliwasilishwa kwenye mtandao mmoja wa Ikulu ya White House na raia mmoja wa Marekani.
Rais wa Marekani hana madaraka ya kuamuru mtu kuondolewa kwa lazima nchini Marekani, na haijabainika iwapo Ikulu ya White House itajibu ombi hilo.
Bwana Justin Beiber amejikuta matatani mara kadhaa na maafisa wa polisi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mapema asubuhi Alhamisi iliyopita, bwana Bieber alikamatwa kwenye Ufukwe wa Miami baada ya afisa mmoja wa polisi kumfumania akiendesha kwa kasi gari la kukodi aina ya Lamborghini rangi ya njano kwenye barabara ya umma.
Akimshuku kuwa alikuwa mlevi afisa huyo alimtia mbaroni.
Kadhalika alifunguliwa mashtaka ya kupinga kukamatwa na pia kuendesha gari akiwa na leseni iliyopita muda wa matumizi.