Dodoma.
Ngumi mkononi ndilo neno jepesi ambalo linafaa kutumika baada ya vurugu kubwa kutokea jana ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi cha kumlazimisha Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina kabla ya wakati wake.
Ngumi mkononi ndilo neno jepesi ambalo linafaa kutumika baada ya vurugu kubwa kutokea jana ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi cha kumlazimisha Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina kabla ya wakati wake.
Semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
imekuwa ikianza saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kabla ya kuendelea
tena kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 3:00 usiku. Jana, katika kipindi
cha asubuhi, semina hiyo iliahirishwa saa 6:17 licha ya kuanza saa tano
asubuhi kabla ya kurejea tena saa 10 jioni.
Ngumi zilitaka kupigwa baada ya Waziri wa Katiba
na Sheria wa Zanzibar, Abubakari Hamis Bakari kuhoji uhalali wa
Christopher Ole Sendeka na Ummy Mwalimu kuchangia wakati hawakuwamo
katika orodha ya wachangiaji jambo ambalo liliibua mjadala mkali na
kurushiana maneno kabla ya Mwenyekiti Pandu Ameir Kificho kuahirisha
semina hiyo.
Chanzo cha vurugu
Kificho alimpa Ole Sendeka nafasi ya kuchangia
Kifungu namba 58 cha rasimu ya kanuni na baada ya kutoa mchango wake,
Hamisi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, alisimama na kumtaka
Mwenyekiti Kificho kuacha kuwateua watu ambao hawamo katika orodha ya
wachangiaji.
Kificho hakumsikiliza na badala yake, alimpa
nafasi mjumbe mwingine wa Bunge hilo Ummy Mwalimu ambaye pia ni Naibu
Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchangia. Hata hivyo kabla hajafanya
hivyo, Bakari alisimama tena na kumzuia kuchangia kwa madai kuwa
hakuwamo kwenye orodha ya wachangiaji.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea na
utaratibu huu suala la kuchangia kanuni linaweza kutupeleka hadi miezi
sita bila ya kumaliza. Haya majina hayakuwemo kwenye orodha ya
wachangiaji na huyo aliyemaliza sasa Ole Sendeka, naye hakuwamo, naomba
tuache mchezo huu,” alisema Bakari.
Aliendelea: “Sekretarieti inakuchomekea majina
mwenyekiti na kama hivyo ndivyo, basi tunatakiwa kuwachukulia hatua kali
hawa kwani tunataka kujadili hoja ambazo hazimo.”
Bakari alisema wajumbe waliotakiwa kuchangia ni
wale ambao walipeleka majina kwa makatibu wa Bunge hilo pamoja na
michango yao kwa maandishi ili wapewe nafasi ya kuzungumza, lakini
Kificho alikuwa akiwateua wajumbe ambao hawamo katika orodha hiyo.
Kificho ajibu
“Mimi sina tatizo na jambo hilo, mkisema tuendelee
basi sawa, lakini mkitaka tufanye mambo kwa uzuri inawezekana pia,
jambo la muhimu ni kuwa tupo hapa kutengeneza Katiba ya wananchi siyo ya
vyama.”
Kelele zilianza kusikika huku wajumbe wakiimba
kuwa mwenyekiti anayumba… na kumtaka mwenyekiti atoke nje na kukiacha
kiti, kwani anafanya upendeleo.
Kelele hizo ziliambatana na wajumbe hao kuwasha vipaza sauti
bila utaratibu. Mjumbe Sadifa Juma Khamis ndiye aliyekuwa wa kwanza
kuwasha kipaza sauti chake na kusimama wakati wote akisema anataka
kuchangia, huku akiungwa mkono na wajumbe wengine kadhaa.
Kutokana na tukio hilo, Kificho alilazimika
kumwita Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu ambaye
alikiri kuwa yako majina ambayo hayakuwamo kwenye orodha, lakini kwa
mwenyekiti yalionekana.
Moto zaidi uliwaka baada ya Ole Sendeka kusimama
hata bila ya kupewa nafasi na kusema anazijua kanuni vizuri na kwamba
asingeweza kuzivunja.
“Nilijua hayo yote na mimi siyo dhaifu wa kanuni
kwani najua kila kitu na tulikwenda tangu mwanzo; mimi, Mheshimiwa Ummy
Mwalimu na Peter Serukamba, ndiyo maana majina yetu yamo humo ila kama
mapigo yetu yanawakwaza wengine waseme, siyo jukumu la mimi kupeleka
mapendekezo yangu kwa Bakari, labda kama wewe una msimamo wako na chama
chako,” alisema Ole Sendeka.
Kauli hiyo ilizusha kelele za wajumbe ndani ya
ukumbi, huku Kificho akiwatuliza na kusema Ole Sendeka aliteleza ulimi
na kumtaka aombe radhi kama anataka, lakini mjumbe huyo aligoma kwa
kuonyesha ishara ya mikono, jambo ambalo lilimfanya Bakari kusimama
tena.
Bakari alisimama na kueleza uzoefu wake wa miaka 34 kwenye Bunge akijisifu kuwa yeye ni zaidi ya Ole Sendeka.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sihitaji kuombwa
msamaha na Ole Sendeka, nimekuwa kwenye mabunge haya tangu mwaka 1980,
leo hii mtu kutoka Simanjiro miaka 10 iliyopita hawezi kunitisha,”
alisema Bakari.
Wengine nusura wapigane
Kauli hiyo iliwafanya wajumbe wengi bungeni
kusimama, huku wengine wakitaka kupigana ngumi baadhi wakisema: “Twende
nje tukapigane, twende nje tukapigane…”
Waliokuwa wakibishana zaidi ni Abdalla Sharia
ambaye alitaka kupigana na Khatibu Haji kabla ya kuzuiwa na wenzao, huku
Tauhida Nyimbo akitaka kuzikunja na Seleman Bungara (Bwege).
Wakati Bunge likiwa limechafuka na kukiwa na
kelele nyingi, mwandishi wa habari hizi alimuona, Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda akimuonyesha kwa ishara ya mikono
Kificho kuahirisha semina.
“Naahirisha semina hii mpaka saa kumi jioni,”
alisema Kificho na kuwafanya wajumbe kupiga kelele huku wengine
wakishangilia na baadhi wakiguna.
Nje ya ukumbi
Wakiwa nje ya ukumbi, Ole Sendeka alisema hoja
zake ni nzito na haziwezi kuzimwa na Bakari ambaye anaonekana kuwa na
masilahi binafsi.
Alisema yeye pamoja na wenzake (Ummy na
Serukamba), bado wanatarajia kuwasha moto kwa kila kifungu ili mambo
yaweze kukaa vizuri na kuwa kilichotokea kwake ni burudani.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
tatizo kubwa lililosababisha mambo hayo ni misimamo ya mwenyekiti
kuyumba wakati wote.
Hata hivyo, alilaani kitendo cha wajumbe wengine
kuwa na hoja alizoziita za kitoto kwa kuzomeazomea akisema hata kama
kiti kinayumba, bado walipaswa kuwa watulivu na kuangalia
kilichowapeleka Dodoma.
Mjumbe mwingine, Charles Tzeba ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Uchukuzi, alitetea kauli ya Sendeka na kusema hata kama
hakuwa kwenye orodha alipaswa kuchangia kwani hiyo ilikuwa ni semina
ambayo kila mtu anayo haki ya kuchangia wakati wowote.
Bunge liliporejea jioni, wajumbe wawili-James
Mbatia na Profesa Mark Mwandosya walisimama na kutoa nasaha za kutuliza
jazba pale wajumbe wanapokwaruzana, huku Mwenyekiti Kificho akisema
kilichotokea asubuhi kilitokana na yeye kutokujua kwamba baadhi ya
wajumbe hawakuwa katika orodha.