Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’.
Exclusive Interview! Staa anayeuza zaidi kwa sasa kwenye muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’ amefungukia skendo ambazo zimekuwa zikimtafuna kila kukicha huku akieleza kuwa, sasa anajuta kuwa staa.
Penny.
Ni kweli unatumia ndumba kutafuta mafanikio?Diamond: “Baadhi ya watu wanakuwa na imani hizo kuwa mimi natumia mambo ya kishirikina kutafuta mafanikio lakini kwa wasiojua ni kwamba kila nifanyalo namtegemea Mungu na muongozo wa mama yangu mzazi (Sanura Kassim a.k.a Sandra).
“Hao ukijumlisha na jitihada zangu mwenyewe na kujituma sana ndiyo wanaonifanya niwe hapa nilipo leo.
“Si kwa sababu ya mambo ya kishirikina. Kwanza siamini katika ushirikina.”
Wema.
Hili la mama Wema Sepetu kudai umemloga Wema likoje?“Sijawahi kumsikia mama Wema akisema nimemloga Wema na hata kwenye magazeti sijaona ila siku nikimsikia ndiyo naweza kusema chochote juu ya hilo.”
Unazungumziaje madai ya wizi wa nyimbo za wasanii wenzako?
Diamond: “Kwa hatua niliyofikia mimi si mtu wa kuiba wimbo wa mtu, bali wapo baadhi ya watu wanaopenda kunisukumia skendo kwa sababu wanazozijua wenyewe.
“Wakati mwingine wanaotuponza ni maprodyuza ambao huenda siku za nyuma walitengeneza biti kali kwa ajili ya msanii fulani, msanii huyo akaingia mitini.
Jokate.
“Siku unakwenda studio kwake anakusikilizisha biti hiyo na ukiiona kali anakuambia uilipie utengeneze ngoma.“Baadaye ndiyo unasikia msanii mwingine anaibuka na kusema kaibiwa biti au wimbo. Sasa hapo kosa ni la nani?
Kwa nini una msururu wa mademu?
Diamond: “Mimi ni Sukari ya Warembo na ni kweli baadhi nilikuwa nao kwenye uhusiano lakini wengine ni maneno ya watu tu, sijawahi kutoka nao.
“Kuna ambao wanajitafutia umaarufu kupitia kwangu kwa kusema nimetembea nao lakini siyo kweli. Si unajua ukizungukwa na uaridi na wewe unanukia uaridi? Ndivyo hivyo, wapo baadhi wanajitangazia tu ili wapate umaarufu.”
Baadhi ya warembo ambao tayari ameshaelezwa kutoka nao kimapenzi ni pamoja na Rehema Fabian, Pendo Maisha Plus, Jacqueline Wolper, Natasha, Najma Shaa, Jokate Mwegelo, Penniel Mungilwa ‘Penny’ na Wema Sepetu.
Unazungumziaje U-freemason wako?
Diamond: “Mimi siamini juu ya imani hiyo kabisa na sijui kama ipo. Huenda mavazi wakati mwingine yanafanya watu wanahisi hivyo. Kama ni mafanikio niliyonayo, yanatokana na kazi zangu za muziki ambazo kila mmoja anaona.
“Naweza kusema napata shoo nyingi ambazo nalipwa pesa nyingi na mimi situmii pesa yangu kwa anasa. Nawekeza ili baadaye mali zinisaidie nitakaposhuka kimuziki. Huwezi kuwa juu muda wote hivyo ni lazima niwe na tahadhari.”
Ni kweli unawapa mademu mimba kisha kuwatosa hivyo wanachoropoa?
Diamond: “Mabinti wanaoibuka na kusema nimewapa mimba ni walewale wanaotafuta umaarufu ‘kick’ kupitia mimi. Ndiyo maana kuna yule aliyeibuka na kuandikwa na magazeti lakini baadaye alikanusha mwenyewe.
“Najiheshimu na namjua Mola, najua kufanya hivyo ni sawa na kuua.”
Kwa mujibu wa Diamond, kumekuwa na baadhi ya wasanii wenzake ambao wamekuwa wakimchonganisha na mastaa wenzake, mfano ukiwa ni hivi karibuni ambapo alizushiwa kumkandia Ali Kiba ili waingie kwenye bifu.