Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimekerwa na kauli ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa , kuwa serikali inaendelea kujadiliana na taasisi za fedha juu ya namna ya kulipa deni la malimbikizo ya mishahara ya walimu yanayofikia Sh. bilioni 61.
CWT imesema kauli hiyo ya serikali ni kutafuta visingizio baada ya
kushindwa kutekeleza ahadi yake kuwa ifikapo Februari, mwaka huu deni la
walimu litakuwa limelipwa.
Rais wa CWT, Gration Mkoba, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema majadiliano ya mishahara ya walimu yalitokana na mgomo wa 2012
baada ya kukaa kwenye meza ya majadiliano na serikali ilikubali kulipa
deni na kuandaa utaratibu wa kupandisha walimu madaraja.
“Inasikitisha kuona majadiliano yanahusisha waandishi wa habari bila ya
kujua kuwa kwa kauli yake waziri tayari walimu wameingia kwenye mgogoro
na serikali, lakini nawasihi walimu wasubiri tamko rasmi la mgogoro,”
alisema.
Mkoba alisema tangu serikali ilipoahidi kutekeleza madai yao, hakuna
hata dai moja lililotekelezwa lakini imewashangaza kuona ikijinadi
kuwa inaendelea na majadiliano ya kulipa deni hilo wakati majadiliano
hayana tija kwa mwalimu.
Alisema Novemba, mwaka jana mkutano mkuu wa CWT ulitoa siku 60 kwa
serikali kukamilisha taratibu zote la kulipa malimbikizo ya mishahara ya
walimu nchini.
Pia Januari mwaka huu kwenye kikao cha Baraza la Taifa la CWT
kiliazimia kuwa ifikapo mwishoni mwa Februari, mwaka huu, ikiwa serikali
itashindwa kulipa malimbikizo hayo litakuwa tayari kuongoza mgomo.