Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana
alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa mapendekezo
yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu kupitisha
baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba.
Katika mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema:
“Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano)
tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba
Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu
kuyatazama. “Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha
inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge
limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa
kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi
huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama
alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania
wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika
Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi
unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika misimamo
inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa
katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge
mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani
na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe
wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
alisema: “Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua njia za aibu, baada
ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe.”
Katika ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro
aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe
kwenye makazi yao na “kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya
kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya
vikao hivyo vya siri.” Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa
Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa
chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri
kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za
kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro
amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha
mahakamani.
“Siwezi kumuacha hivihivi Mtatiro, lazima nichukue hatua. Hawa
niliwaalika kama marafiki tu, tukala wote chakula. Mbona hata kesho
nimealikwa na Kajubi Mukajanga (Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Tanzania), hivi nikienda kukutana naye ndiyo atakuwa amenipa rushwa?”
Waziri mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa kwa
sababu hakupatikana kujibu tuhuma zake anadaiwa kuwaalika wawakilishi
wa vyuo vya elimu ya juu, huku mbunge mmoja pia akidaiwa kuwaita
wafugaji.
Kulikuwa na mgawanyiko wa wazi katika kanuni hiyo
ya upigaji kura, CCM kikitaka kuungwa mkono kwa utaratibu wa kupiga kura
za wazi huku wapinzani wakitaka za siri kama zilivyokuwa zimependekezwa
na Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni.
Akizungumzia suala hilo, Mjumbe wa Bunge hilo,
Makersia Jibubu alisema: “Sikutarajia haya. Nilichojua, tungefika wiki
ya kwanza tukapitisha kanuni na baada ya hapo tukaendelea na mijadala.
Lakini kinachoonekana ni mivutano ya wanasiasa na kibaya zaidi wote
wanalenga kundi la wajumbe wateule wa Rais.”
Alisema alianza kuwa na wasiwasi kuhusu Bunge hilo, mara tu
alipofika na kundi lake kuitwa na moja ya vyama vya siasa kufanya
mazungumzo kwa lengo la kutaka ushawishi wao.
“Makundi yote yaliyoteuliwa na Rais yaliitwa na
vyama vya siasa. Wakaandaa mikutano kwa chakula na vinywaji, halafu
wakaanza kueleza sera zao. Nikasema sasa hii ni kwa faida ya nani?”
Mkutano wa CCM
CCM kilifanya mkutano wa wajumbe wake juzi usiku
chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Idd. Pamoja
na mambo mengine, kinadaiwa kutoa msimamo kuwalazimisha wajumbe wake
kuunga mkono kura ya wazi.
Chama hicho kilitumia takriban muda wa saa tatu
kuwafunda wajumbe hao ili kuhakikisha kuwa wanatetea utaratibu huo.
Mkutano huo ulianza saa 2:15 hadi saa 5:00 usiku.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidokeza kuwa ajenda kuu ilikuwa ni kupitia rasimu ya kanuni.
Mjumbe mmoja alisema: “Inavyoonekana sasa suala la
kupiga kura ya wazi ni amri na halina tena mjadala, lakini litaleta
matatizo makubwa mbele ya safari… yetu macho.
“Mle ndani sisi wengine tuliamua kunyamaza kimya, maana hata unaposimama na kuchangia bado watu wanakuona kama ni msaliti.”
Wakati wa semina ya wajumbe kuhusu rasimu ya kanuni, wajumbe
wawili kutoka CCM, Ester Bulaya na Profesa Juma Kapuya waliweka wazi
kuwa wanaunga mkono kura za siri, huku Anna Kilango akisema suala la ama
kupigwa kura ya wazi au ya siri liamuliwe kwa kura ya siri kwa kuwa
limezua mvutano.
Kikao cha Ukawa
Katika hatua nyingine, wapinzani na wajumbe wa
makundi mengine ya kijamii chini ya Umoja wao wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), walikutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa na kuweka msimamo wa
kupinga kura ya wazi kwa nguvu na gharama zozote.
Mmoja wa wajumbe wake, John Mnyika alisema uamuzi
mwafaka ni kura ya siri kuamua vifungu mbalimbali vilivyomo katika
Rasimu ya Katiba. Mjumbe Tundu Lissu alisema: “Hatutakubali zipigwe kura
za wazi, sisi bado tumesimamia palepale.”
Sitta na Suluhu wapitishwa
Habari zilizopatikana jana jioni zinasema wajumbe
wa Bunge hilo wa CCM walikutana na kuwapitisha Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi za uenyekiti na
makamu mwenyekiti’.