KAMATI ya Uongozi ya Chama Cha Mapinduzi ( C C M ) imempitisha Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kwa kauli moja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
Pia kamati hiyo imempitisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo.
Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo ya uongozi ya CCM iliyoketi jana, zimebainisha kuwa Andrew Chenge aliyekuwa akitajwa kuwania nafasi ya Mwenyekiti, amejitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa hiari yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kanuni za Bunge kupitishwa, utaratibu wa kuchukua fomu utatangazwa ambapo Sitta atakwenda kuchukua na atakuwa mgombea pekee kutoka CCM.
Kitakachosubiriwa ni kuona wagombea kutoka makundi mengine kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo na kundi linalotarajiwa ni kutoka vyama vya siasa vya upinzani.
Sifa za Sitta
Sifa ya kwanza imetajwa kuwa ni utayari wake katika kuliongoza Bunge hilo.
“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imeainisha sifa za mtu anayetakiwa kuwa Mwenyekiti na mimi nina sifa na nina mipango mizuri ya kuwafanya Watanzania wapate Katiba bora kama ndoto ya Rais wetu (Jakaya Kikwete) ilivyo,” alinukuliwa Sitta akizungumzia nia yake.
Kisheria, sifa za mtu anayepaswa kuongoza Bunge hilo ni pamoja na kuwa na Shahada ya Sheria kutoka katika chuo kinachotambulika, pia kuwa na uzoefu wa kuendesha mijadala kama ya Bunge.
Sitta anatajwa kuwa na sifa za kushika nafasi hiyo, ikiwemo uzoefu wa miaka mitano wakati alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inaelezwa kuwa katika Bunge hilo la Tisa wakati akiwa Spika, mijadala mizito ilijadiliwa lakini hakutetereka hata kidogo. Waziri huyo pia amekuwa akitajwa na wapambe wake kuwa anafaa kuwania nafasi ya uenyekiti kwa sababu uadilifu wake hauna shaka.
Mbali na uadilifu na uzoefu wake katika uongozi wa Bunge aliloliita la kasi na viwango, inadaiwa hata makundi mengine, wakiwemo wabunge wa upinzani na asasi za kiraia, wanamkubali.
Mwenyewe Sitta aliwahi kunukuliwa akieleza sababu ya kukubaliwa na wabunge wa upinzani kuwa wanaamini akikalia kiti hicho, ataendesha Bunge hilo kwa misingi ya uwazi na haki.
Sifa ya nyingine anazotajwa nazo, ni uwezo wa kutumia busara kukabiliana na makundi yenye maslahi mbalimbali na kuwaleta pamoja.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo tayari wanamuona Sitta kuwa mjumbe pekee mwenye uwezo huo, kutokana na uzoefu mdogo uliopatikana katika wiki mbili za Bunge hilo Dodoma.